Tuesday, 24 March 2020

MWAKA WA KI-ROHO KWA WALEI


MWAKA WA KI-ROHO KWA WALEI

Kwa nini kwanzisha mwaka wa ki-roho?

Wakati wa karne ya 20 Mungu alitujalia neema nyingi. Mojawapo ndiyo Upyaisho wa Roho Mtakatifu. Mwaka 1967, miaka miwili tu baada ya Mtaguso wa Vatican II, kikundi cha Wakatoliki, huko Marekani,  walionja ‘Ubatizo wa Roho Mtakatifu’, yaani nguvu na karama zake. Tangu siku ile mamilioni wa Wakatoliki walijazwa Roho Mtakatifu, kuongozwa naye, kuwezeshwa naye kueneza Habari Njema ya Yesu Kristo na kuishi Injili kwa furaha. Baadhi yao vijana wengi wamejitoa, kwa moyo wote, kufanya kazi ya utume.

Lakini baada ya miaka kadhaa, wengi wanaanza kukata tamaa wanapokutana na majaribio, matatizo, n.k., hasa wakionja ukame wa ki-roho. Wanafikiri kwamba Mungu amewaacha. Basi wanaacha kazi ya utume. Wengine wanajaribu bahati yao kwa kujiunga na makanisa mengine ya ki-pentekoste. Wengine wanaacha hata kuishi maisha yao ya kikristo wakisema moyoni: "Nimedanganywa".

Mimi binafasi nafikiri kwamba kuna sababu nyingine. Shina la matatizo ni kukosa misingi wa maisha ya ki-roho. Mkristo hawezi kuwa mtume wa kudumu bila kuimarishwa ki-roho. Imani yake isibaki kichwani kama elimu bali iongoze matendo yote ya maisha yake. Tena imani isitegemee hisia zake, bali hisia zake zitawaliwe na imani yake. Wengi baadhi ya vijana waliojitoa kwa Mungu wanabaki katika mang’amuzi ya ‘Ubatizo wa Roho Mtakatifu’ na hawaendi mbele katika safari zao za ki-roho. Ni muhimu sana kukutana na Yesu Mfufuka na kwa namna nyingine ni lazima, lakini ‘experience’ hiyo ni mwanzo wa safari ya Mkristo.

Yesu alikaa Nazareti miaka 30 kabla ya kubatizwa katika Roho Mtakatifu, na baada ya kubatizwa katika maji na Roho alienda tena jangwani muda mrefu kutafakari ‘experience’ hiyo, kabla ya kuanza
kuhubiri hadharani na kuwaombea watu. Paulo, baada ya ubatizo wake, alienda katika nchi ya Arabuni kwa miaka mitatu, kabla ya kutangaza huko Dameski, kwa muda mfupi, kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu. Na baadaye alikaa Tarso miaka mingi kabla ya kutumwa na Roho Mtakatifu kutangaza Habari Njema ya Yesu kwa Wapagani wote, (Gal 1:15-24). Mungu anahitaji muda kumtayarisha mtu awe chombo kiteule mikononi mwake.

Kutokana na maelezo hayo hapo juu, ndiyo maana tumeanza Mwaka wa ki-roho kwa walei. Mafundisho yanalenga waliomtolea Yesu maisha yao lakini bado wana kiu ya kujiendeleza ki-roho.

Makusudi ya Kituo hiki ni kujenga misingi ya maisha yao ya ki-roho, kwa njia ya kazi, sala na mafundisho, na nidhamu ya maisha ya kawaida. Kinawakaribisha hasa Vijana, wavulana kwa wasichana,- hata watu wazima - wanaotaka kujifunza zaidi, kwa muda wa mwaka mmoja, misingi ya maisha ya ki-roho, kukua katika imani yao ya ki-katoliki, kujijengea nidhamu kwa maisha ya mbele na kudumu katika huduma zao.

Licha ya sala na mafundisho wanafunzi wanajizoesha kwa njia mbalimbali, kama kwa mfano, kazi ya mikono, kutafakari porini uumbaji wa Mungu, matembezi kwa miguu (Tazama: Walking in the footsteps of the missionaries of the first caravan, 1878-1879), na kufurahi pamoja.

Idadi ya wanafunzi
Kituo hiki ni kichanga. Kila mwaka, mwezi wa Julai, tunawapokea wanafunzi wapya. Mwaka 2009-2010 tulipokea wanafunzi 10. Mwaka 2010-2011 wanafunzi 7. Mwaka 2011-2012 wanafunzi 12, kwa Mwaka 2012-2013 tulipokea pia wanafunzi 12. Kwa mwaka huu 2019-2020 tumepokea wanafunzi 21.

 Hakuna malipo.

Mtu hatalipa ada, wala hatalipwa, bali atafanya kazi asubuhi kutimiza amri ya Mungu: "Kwa jasho la uso wako utakula chakula", Mwa 3 :19. Mchana atafundishwa, atapata nafasi ya kusoma Neno la Mungu na kukaa kimya mbele ya Mungu Baba: "Ingia katika chumba chako cha ndani na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini", Mt 6:6.





Ombi la kujiunga na Shule



Kujiandikisha

Yeyote anayetaka kujiunga afadhali ajaze fomu, iliyochapisha chini na aitume kwa anwani iliyoandikwa katika fomu hiyo.





Anayestahili kujiunga na Shule
  Makusudi ya Kituo cha Kungwe ni kujenga misingi ya maisha ya ki-roho ya Wakristo, kwa njia ya kazi, sala, mafundisho na nidhamu ya maisha. Kituo hiki kinalenga Wakarismatiki tu waliomaliza semina ya maisha ya ki-roho na semina ya makuzi, waliomtolea Yesu maisha yao lakini, bado wana kiu ya kujiendeleza ki-roho. Kinawakaribisha hasa Vijana, wavulana kwa wasichana (umri si chini ya miaka 21), - hata watu wazima (umri isiyozidi 50) - wanaotaka kujifunza zaidi, kwa muda wa mwaka mmoja, misingi ya maisha ya ki-roho, kukua katika imani yao ya ki-katoliki, kujijengea nidhamu kwa maisha ya mbele na kudumu katika huduma zao.
Kituo hiki ni kichanga. Tunaweza kupokea watu 18 hadi 20 tu, wanaume 12 na akina dada 8.

 Ukubali masharti ya kujiunga na Shule
Hakuna malipo. Hutalipa ada, wala hutalipwa, bali utafanya kazi asubuhi kutimiza amri ya Mungu: "Kwa jasho la uso wako utakula chakula", Mwa 3:19. Mchana utafundishwa, utapata nafasi ya kusoma Neno la Mungu na kukaa kimya mbele ya Mungu Baba: "Ingia katika chumba chako cha ndani na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini", Mt 6 :6. Kila mwezi utaweza kwenda jangwani kukaa peke yake mbele ya Mungu kati ya viumbe na kumsikiliza.
Tunaomba T.shs 100.000/- ziwe akiba yako kwa ajili ya matibabu. Kama una bima fika na bima yako, lakini fedha itahitajika bado kwa ajili ya usafiri.


No comments:

Post a Comment